Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul Bayt (a.s) – ABNA, Rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel, alisema hayo leo Jumapili wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika mjini Havana kwa wito wa Chama cha Kikomunisti kinachotawala nchini humo.
Akihutubia maelfu ya waandamanaji, Díaz-Canel alisema:
“Enyi mataifa ya Amerika, njoni tuunganishe safu zetu.”
Alilaani vikali shambulio la kinyama la Marekani dhidi ya Venezuela pamoja na kitendo alichokitaja kuwa ni utekaji nyara usiokubalika na wa kikatili wa Rais Nicolás Maduro.
Rais huyo wa Cuba alisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kupuuza athari hatari za vitendo hivyo vya kihalifu kwa amani ya kikanda na ya dunia kwa ujumla.
Katika maandamano hayo, waandamanaji walipaza sauti kaulimbiu ya “Kifo kwa Ubeberu”, huku wakipeperusha bendera za Cuba na Venezuela kuonesha mshikamano wao.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema kuwa serikali ya Havana inapaswa kuwa “na wasiwasi” kufuatia kukamatwa kwa Maduro. Tangu kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House, mashinikizo dhidi ya Cuba yameongezeka, na taifa hilo limeorodheshwa tena katika orodha ya Marekani ya kile kinachoitwa “nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi”.
Kwa sasa, Cuba inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, hali inayochangiwa na vikwazo vya Marekani pamoja na udhaifu wa miundombinu ya kiuchumi. Uhaba wa fedha za kigeni na mafuta umesababisha kupungua kwa uzalishaji wa umeme na kudorora kwa shughuli za kiuchumi nchini humo.
Hatua hizi zinajiri huku Marekani ikitangaza rasmi kukamatwa kwa Nicolás Maduro na mkewe, pamoja na kuhamishwa kwao kwa njia ya anga hadi nchini Marekani, jambo lililosababisha wimbi la hisia, mijadala na lawama kali katika ulingo wa kimataifa na mitandao ya kijamii.
Your Comment